HAPO KATIKATI YA KAPIRIMPOSHI NA DAR ES SALAAM KUNA NINI?

March 29, 2022
Blog, Visual Arts in Tanzania

Imeandikwa na Fred Halla

Safari ni Safari, haijalishi unatembea kwa miguu, unatumia baiskeli, motokaa, jahazi, ndege au gari moshi la msingi ni kuwasili kule uendako. Kuna wakati unaweza fika salama lakini njiani kukawa na misuko suko ya hapa na pale mfano dhoruba, hitilafu, maradhi na rabsha kadha wa kadha. Ukiachana na Safari pamoja na njia mbali mbali za kufanikisha safari, kuna huyu msafiri ambaye anatoka eneo moja na kuelekea eneo lingine kwa kutumia njia mojawapo ya usafiri uliotajwa hapo juu.

Mara nyingi safari huja na simulizi kadha wa kadha, zenye kufurahisha, kupendeza, kusikitisha na pengine za kutisha. Leo hii ningependa kuongelea kwa kifupi tu juu ya safari ya msanii Klaus Hartmann kutoka Ujerumani ambaye alisafiri toka Zambia kuja Tanzania, akitokea Kapirimposhi kuja Dar Es Salaam, hakuja tu kutembea bali ni kwa mualiko maalum kutoka taasisi ya Sanaa inayoongoza nchini Tanzania, Nafasi Art Space ili atushirikishe akijuacho naye kujifunza asichokijua. Kila mwaka Nafasi Art Space hutoa nafasi kwa wasanii mbali mbali kutoka ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania kutumia muda wa mwezi mmoja au Zaidi kwa msanii kufanya kazi ya Sanaa na hatimaye kuionyesha kwa hadhira. Kama nilivyoelezea hapo mwanzo kuwa kila safari ina hadithi yake, basi ndivyo ilivyo kwa Bwana Klaus ambaye katika safari yake alitumia usafiri wa Gari Moshi kwa reli ya TAZARA (ushirikiano wa usafiri wa reli kati ya Tanzania na Zambia) alikuwa na jambo la kutusimulia. Kama ilivyo kwa wengi tunaposafiri njiani kuna mambo na vitu mbali mbali ambavyo hatutilii maanani na kuvichukulia ni vitu vya kawaida. Lakini kwa Klaus Hartmann vitu hivyo vya kawaida kwake yeye ni hadithi nzuri ambayo ameweza kuisimulia vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu kupitia michoro ya rangi.

Kama wewe ni msafiri wa kutumia Gari moshi (Treni) au basi utakuwa shahidi kuwa kuna vitu au mambo yanayotokea ukiwa safarini, na unaona vitu vingi vya kuvutia na vingine visikuvutie, Klaus katika safari yake ameweza kutukusanyia taarifa mbali mbali kama vile aina za nyumba za wenyeji, nyumba zilizo katika miundo na mpangilio tofauti wa kuvutia, nazo zimejengwa pembezoni kufuata njia ya reli. Katika baadhi ya maeneo Bw. Klaus amevutiwa na shughuli za kiuchumi na jinsi wenyeji wanavychangamkia fursa ya uwepo wa Reli ya TAZARA. Biashara kama vile Vyakula, vikapu na Matunda ya aina mbali mbali. "Haikuwa rahisi kwangu kupata kila picha niliyoitaka kwa kuwa treni ilikuwa iko katika mwendo, alisema Klaus, "...Lakini kila iliposimama niliweza kupata nafasi ya kukusanya taarifa zilizonisaidia katika kazi yangu", aliongeza. Ukitazama kwa jicho la kawaida jambo alilofanya Bw. Klaus unaweza kuona ni la kawaida lakini ukitazama na kutafakari ni jambo kubwa na muhimu kwa leo n ahata kwa siku zijazo kwa kuwa michoro yake itadumu kwa miaka mingi ambapo mabadiliko haya ya kasi yanayoendelea baadhi ya taswira hazitakuwepo lakini kwa kupitia Klaus zitakuwepo.

Klaus Hartmann ni msanii kutoka Ujerumani aliyekuja mpango wasanii waalikwa kutoka nje ya Tanzania unaoendesha na kuratibiwa na kituo cha Sanaa cha Nafasi Art Space. Hii si mara ya kwanza kuzuru Afrika Mashariki, na ameandika na kuchapa vitabu kadhaa vyenye majengo na mandhari mazuri ya vijiji kutoka nchi za Tanzania, Rwanda na Zambia.